Wednesday, April 5, 2017

Uzinduzi wa Ugawaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa watumishi wa Serikali Ukerewe.

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Estominh F. Chang'ah akipokea kitambulisho cha Taifa kama ishara ya Uzinduzi wa ugawaji wa vitambulivyo hivyo akiwa na Shahidu D. Mrabyo.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Estominh F. Chang’ah amezindua rasmi zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa watumishi wote wa Serikali walio andikishwa Wilayani Ukerewe. Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi mkubwa wa Halmashauri ambapo amepongeza zoezi limefanikiwa kwa asalimia 97%. Kitambulisho kitarahisha huduma mbalimbali na kuongeza maendeleo na kupunguza urasimu na itasaidia hata kwa watumishi watakao hitaji mikopo ya kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo. 

Shahidu D. Mrabyo Afisa Msajili (W) akiongea na watumishi wakati wa Uzinduzi
Shahidu D. Mrabyo Afisa Msajili (W), ameeleza kuwa zoezi la uandikishaji lilianza tarehe 3/4/2016 na Katika zoezi hilo jumla ya watumishi waliotakiwa kusajiliwa ni 3103 lakini watumishi 2932 walitambuliwa na kusajiliwa na maafisa wa NIDA kwa kushirikiana na Uongozi husika wa mashirika au Taasisi za serikali, na watumishi 81 walikua tayari wamekwisha sajiliwa sehemu mbalimbali nchini na hivyo kufanya idadi ya wanaotakiwa kuwa na vitambulisho kuwa 3013 na hivyo kufanya zoezi hili kufanikiwa kwa 97.099%.
Watumishi wa Serikali katika ukumbi wa  Halmashauri wakati wa uzinduzi 
Vitambulisho vinatengenezwa kwa awamu mbili, vitambulisho 2932 vilivyoombwa, kwa awamu ya kwanza ni vitambulisho 2519 vipo tayari kwa kugawiwa sawa na asilimia 85.91 na vilivyobaki vitakuja katika awamu nyingine.
Kitambulisho cha Taifa kina uwezo mkubwa wa kufanya kazi nyingi kwa pamoja, huko tunako elekea katika teknolojia kitatumika kama kitambulisho cha Taifa, kitatumika kupigia kura, kitatumika kama kadi ya mfuko wa hifadhi ya jamii, leseni ya udereva, passport ya kusafiria, pia itakuwa ni kadi ambayo unaweza kuhifadhia fedha na kuitumia popote kwa kuchanja tu, pia inaweza kutumika kama kadi ya kuingilia uwanjani mf. Uwanja wa Taifa, tutaweza kuitumia kupanda magari ya mwendo kasi na matumizi mengine mengi kulingana na kadri itavyokuwa inaunganishwa na mifumo mbali mbali hapa nchini.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Song'ora J.K Nyango akipongeza hatua ya ugawaji wa vitambulisho kwa Watumishi wa Serikali
Zoezi linalofuata na ambalo limekwisha anza ni uandikishaji wa wananchi wote ambapo mpaka sasa fomu za usajili zimekwisha sambazwa katika kata zote za Tarafa ya Mumbuga ambazo ni Bukongo, Nkilizya, Kagera, Nansio, Kakerege, Nakatunguru, Bukanda, Namagondo na Ngoma. Ametoa rai kwa wakazi wote wa tarafa ya Mumbuga kwenda kuchukua na kujaza fomu na kuwa na viambatanisho vingi iwezekanavyo ilikurahisisha upatikanaji wa kitambulisho, viambatanisho vinavyohitajika ili kusajiliwa ni cheti cha kuzaliwa, vyeti vya elimu, kitambulisho cha kupiga kura, kitambulisho cha bima ya afya, kitambulisho cha mfuko wa hifadhi ya jamii, TIN namba, kopi ya kitambulisho cha taifa cha mzazi.
Kuhusu mwanachi atakayepoteza kitambulisho cha Taifa atalazimika kulipia Tshs. 20,000/= kwa ajili ya kupata kingine, pia tunatarajia kuanza kusajiri wageni wanaoishi kihalali katika maeneo yetu, kwa hiyo ni vyema kama wapo wakaja kutuona kwa ajili ya kusajiliwa kama wageni.
Mrabyo amemshukuru Mkuu wa Wilaya, Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, wakuu wa idara mbalimbali, wakuu wa taasisi mbalimbali za Serikali na watumishi wote wa Serikali Wilayani Ukerewe.
Shahidu D. Mrabyo akimkabidhi kitambulishi cha Taifa Hakimu Mfawidhi (W) Francis Kishenyi
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe na baadhi ya wakuu wa idara na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya katika picha ya pamoja.


No comments:

Post a Comment