Thursday, March 23, 2017

Wananchi watakiwa kuwa sehemu ya miundombinu bora ya Elimu.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Frank S. Bahati akizungumza na Serikali ya Kijiji,Kamati ya Shule ya Msingi Musozi na baadhi ya wazazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Frank S. Bahati amefanya ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa vyoo katika shule zilizokuwa zimefungwa na kuwasihi wananchi kuwa sehemu ya maendeleo ya elimu katika wilaya ya Ukerewe. Alikutana na Serikali ya kijiji na kamati za shule.


Mkurugenzi Mtendaji wa H/W  Frank S. Bahati Ukerewe akizungumza wa Wazazi na Kamati ya Shule Muhande.
Alitembelea shule tatu ambazo zinaendelea na ukamilishaji wa ujenzi vyoo ambazo ni Shule ya msingi Musozi, shule ya msingi Muhande, na shule ya msingi Malegea. Ujenzi wa vyoo upo katika hatua mbalimbali za kuridhisha ukilinganisha hali iliyokuwepo awali. Shule ya Msingi Musozi iliyopo kata ya Bukindo ujenzi ukikamilika kitakua ma matundu 14 ambapo kimegharimu shilingi 4,425,000/- ambapo fedha za wananchi ni shilingi 776,000/-, Shule ya Msingi Muhande iliyopo kata ya Murutunguru inatarajia kukamilisha matundu 16, Shule ya Msingi ya Malegea iliyopo kata ya Namagondo imekamilisha ujenzi wa matundu zaidi ya 16.

Ametoa agizo kwa Idara ya Elimu Msingi kuwa shule zote zilizofungwa walimu waandae na waanze masomo ya ziada kwa kipindi cha likizo hasa madarasa ya mitihani hii itawasaidia wanafunzi kusoma na kufidia muda uliopotea shule zilipokuwa zimefungwa. Pia amewataka Idara ya Elimu Msingi kufanya uchambuzi wa maeneo yote yenye uhitaji wa kuanzisha shule nyingine ili kukabiliana na wingi wa wanafunzi katika baadhi ya shule.

Mkurugenzi Mtendaji H/W ya Ukerewe akishiriki kazi wa ujenzi wa choo shule ya Msingi Muhande.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Frank S. Bahati  pamoja na baadhi ya watumishi wa Halmashauri wameshiriki  ujenzi wa choo katika Shule ya Msingi Muhande kwa kubeba matofali, mawe na kuchimba msingi vya vyoo hivyo pamoja na wananchi wa Muhande.

Mkurugenzi Mtendaji H/W ya Ukerewe akishiriki kazi wa ujenzi wa choo shule ya Msingi Muhande.

Bahati amewataka wananchi kuwa wazalendo na kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo na kuachana na itikadi tofauti za watu bali kujihusisha na mabadiliko ya elimu Wilayani. Shule zikiwa na upungufu wa miundombinu rafiki na muhimu kwa wanafunzi itawaweka mahali pabaya watoto hivyo jamii ijihusishe na kuwasaidia wanafunzi ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao.“Jukumu la kuleta maendeleo ya shule na elimu kiujumla sio la Serikali pekee bali ni letu wote, kila mmoja awe chachu ya mabadiliko”, alisema Bahati. Wanafunzi wote wanaendelea na masomo na ukamilishaji wa ujenzi wa vyoo katika shule 11 zilizokua zimefungwa unaendelea.

Baadhi ya wazazi wakishiriki Ujenzi wa choo Shule ya Msingi Muhande

Choo kilichokamilika shule ya Msingi Malegea

Mkurugenzi Mtendaji H/W Ukerewe akiwa na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Malegea

Choo Shule ya Msingi Musozi

No comments:

Post a Comment