Wednesday, October 26, 2016

MKURUGENZI MTENDAJI UKEREWE AMEKUTANA NA WATUMISHI WALIOKO OFISI ZA MAKAO MAKUU UKEREWE



Kutoka kushoto ni Kaimu Mweka Hazina(W) Baraka Munuo,katikati ni Mkurugenzi Mtendaji Mhe. Frank Bahati kushoto kwake ni Afisa Utumishi Pelagia Sogoti na Afisa Ardhi na Maliasili Song'ora Nyango.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ukerewe Frank Bahati amewataka watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kufanya kazi kwa bidii kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma na kuhimiza uwajibikaji wa kila mtumishi kwa nafasi yake.
Bahati ameyasema hayo alipofanya kikao na watumishi walioko ofisi za makao makuu ya Ukerewe katika Ukumbi mkubwa wa mikutano wa Halmashauri, ambapo amesisitiza kuwa watumishi wote kuanzia Wakuu wa Idara, Vitengo na watumishi wote kufanya kazi kwa bidii na uadilifu mkubwa na kuondokana na kufanya kazi kwa mazoea. Nanukuu “wakati wa kufanya kazi kwa mazoea umekwisha, kila mmoja kwa nafasi yake ahakikisha anajituma kwa bidii na sio vinginevyo” alisema Bahati.
Baadhi ya Watumishi wa Makao Makuu Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe


Baadhi ya Watumishi wa Makao Makuu Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe
Bahati amehimiza kuwepo kwa ushirikiano baina ya wafanya kazi kwani itasaidia kuleta mahusiano mazuri na kuongeza ufanisi kazini. Ushirikiano ni jambo la muhimu na watumishi wote wafanye kazi bila kuwa na matabaka. Kila Mkuu wa Idara ahakikishe watumishi wote walio chini yake wana mahusiano mazuri ili kuweza kuwahudumia wananchi wa Ukerewe kama inavyopaswa.
Ofisi ya Mkurugenzi kupitia Idara ya Ardhi na Maliasili kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya imeanzisha dawati la malalamiko ambalo wananchi wa Ukerewe wanafika kwaajili ya kueleza malalamiko walionayo ili kuweza kupewa ufumbuzi wa matatizo yao ya ardhi. Mpaka sasa ni malalamiko 35 yameshasikilizwa kupitia dawati la malalamiko ya Ardhi  na walalamikaji kupewa majibu juu ya malalamiko yao. Dawati hilo linakaa kila siku ya Jumanne katika Halmashauri ya Ukerewe Idara ya Ardhi na Maliasili. Bahati amewataka Wakuu wote wa Idara wenye migogoro ya ardhi katika maeneo yao kuyaainisha na kuleta taarifa juu ya migogoro hiyo kabla ya tarehe 30/10/2016 ili Idara ya Ardhi iweze kushughulikia.

No comments:

Post a Comment