Tuesday, April 25, 2017

Visiwa Kumi Wilayani Ukerewe kupata Umeme.


Mkurugenzi Mkuu wa Rex Energy Bw. Francis Kibhisa akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa umeme jua kisiwa cha Gana
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Bw. Frank S. Bahati akizungumza katika uzinduzi wa umeme jua kisiwa cha Gana.
Wananchi wanaoishi maeneo ya visiwani wilayani Ukerewe wanatarajia kunufaika na huduma ya nishati ya umeme. Nishati hiyo ya umeme jua inayowezeshwa na mwekezaji Rex Energy ambao unatakuwa ni moja ya kichocheo cha uchumi wa maeneo mengi ya visiwa katika wilaya ya  Ukerewe na hii ni baada ya kufanya uzinduzi wa mradi huo wa umeme katika kisiwa cha Gana, uliohusisha wananchi waliojitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo lililoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Frank S. Bahati na Mkurugenzi mkuu wa Rex Energy Francis Kibhisa ambaye ndio mwekezaji.

Uwekaji saini katika uzinduzi wa mradi wa umeme visiwani.
Utekelezaji wa mradi wa nishati ya umeme jua unatakuwa wa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza imeanza agosti 2016 na kukamilika  desemba 2017, ambapo miundombinu imefikia hatua nzuri na visiwa vitakavyo nufaika na awamu hiyo ni Gana, Bwiro, Kamasi, na Bulubi. Katika awamu ya pili mradi utakamilika mwaka 2018 ambapo na kunufaisha visiwa vya Kweru kubwa, Kweru mto,Siza, Bushingere, Izinga na Sizu.
Ukaguzi wa miundombinu inayotumika katika mradi wa umeme jua

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Frank S. Bahati ameshukuru Rex Energy kwa kuwekeza nishati ya umeme jua katika visiwa kumi vya Ukerewe. Kupatikana kwa umeme katika maeneo ya visiwa utasaidia kukuza uchumi hasa wa viwanda kwani ni adhma ya serikali ya awamu ya tano kuwa na uchumi wa viwanda. Umeme utawasaidia vijana kujishughulisha na kazi mbalimbali, pia mradi utakua msaada kwa shule,vituo vya afya na taasisi za kidini. Amewataka wananchi kuupokea kwa mikono miwili mradi na kushirikiana kuutunza kuhakikisha unakuwa msaada kwa vizazi na vizazi.
Kikundi cha ngoma kikiburudisha katika uzinduzi wa umeme jua Gana
Mkurugenzi mkuu wa Rex Energy Francis Kibhisa ameshukuru Serikali kuanzia Wizara ya Nishati na Madini, Rea na serikali ya Wilaya ya Ukerewe kwa kutoa ushirikiano wa kufanikisha mradi huo kuanza kufanya kazi katika visiwa vya Ukerewe, baada ya miezi miwili umeme utakuwa umewashwa. Baada ya mradi kuanza kazi kuna maeneo ambayo itashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe kuboresha maeneo makuu matatu ambayo ni Elimu na kuimarisha majengo ya shule na vyoo kama ambavyo wamesaidia ujenzi wa choo cha shule ya msingi Miti mirefu, Afya kuanzisha kituo cha afya au zahanati, usalama kuweka kituo cha polisi.
Moja ya miundombinu ya mradi wa umeme jua kisiwa cha Gana
 “Gharama za mradi ni bilioni 18 hadi 21 ambazo ni sawa dola milioni 9 hadi 11 za kimarekani” alisema Kibhisa. Mradi utakuwa wa manufaa zaidi kwa vijana wengi watapata mafunzo na kuajiriwa katika kazi mbalimbali za Rex Energy. Ametoa rai kwa watanzania kuwekeza ndani ya nchi kama alivyofanya yeye na kuwa maendeleo ya nchi yanaletwa na watanzania wenyewe na kutokata tama katika kusaidia serikali.
Umeme jua wa Rex Energy unatarajiwa kuwanufaisha wananchi zaidi ya 5000 na itavutia wafanyabiashara wengi kutumia fursa na kujiongezea pato na wametakiwa kushirikiana na mwekezaji kutunza miundombinu.

Thursday, April 6, 2017

Ukerewe yashika nafasi ya 24 katika kampeni ya kitaifa ya Usafi na Mazingira


Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe imekua ikishiriki katika kampeni mbalimbli za Usafi wa Mazingira. Kampeni hii imefanikiwa kutokana na ushirikiano baina ya wadau mbalimbali pia kwa kuzingatia Sheria ya Managementi ya Utunzaji wa Mazingira N0. 20 ya 2003. Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe inaendelea na uboreshaji wa Usafi wa Mazingira kwa kufanya usafi katika maeneo mbali mbali. Zoezi hili linafanikiwa kwa kufanya kuwa na kampeni ya Usafi kila mwisho wa mwezi kwa kushirikisha jamii nzima.
KWA PAMOJA TUYATUNZE MAZINGIRA YETU!

Wednesday, April 5, 2017

Ulinzi na Usalama wa Mtoto

Wambura L. Kizito Mratibu wa Ustawi (M) akitoa mada wakati wa kikao kazi
Mtoto ana haki ya kulindwa na kutetewa pale anapotendewa ukatili ni wito uliotolewa na Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mwanza Wambura L. Kizito katika kikao kazi cha Ulinzi na usalama wa mtoto ambacho kimefanyika katika ukumbi wa hospitali ya Wilaya ya Ukerewe na kimewaweka meza moja wadau kutoka makundi mbalimbali wenye wajibu wa kumlinda mtoto kama maafisa ustawi, mwendesha mashitaka, hakimu mfawidhi, polisi, viongozi wa dini, NGO’s, wawakilishi wa watoto,idara ya maendeleo ya jamii, idara ya elimu msingi na sekondari na idara ya afya.
Washiriki wakisikiliza mada
Watoto hukumbana na ukatili mbalimbali katika maeneo mbalimbali wanapokuwepo, baadhi ya ukatili wanaokutana nao watoto ni pamoja na ukatili wa kihisia ambapo mtoto anakutana na matusi, kinyimwa chakula, kuto thaminiwa, ukatili wa kimwili inaambatana na vipigo,kukatwa viungo vya mwili, kuchomwa moto, kutumikishwa, ukatili wa kingono inahusisha kubakwa, kulawitiwa, kuguswa maeneo binafsi, kunajisi na ndoa za utotoni.
Wambura L. Kizito Mratibu wa Ustawi (M) akitoa mada wakati wa kikao kazi
Lengo la uwezeshaji ni kuhakikisha mtoto analindwa na Halmashauri inanafasi ya kuweka mifumo madhubuti ambayo itamtunza na kumthani mtoto na kufuata sera, kanuni na taratibu mbalimbali za kumlinda mtoto na zitasaidia kukabiliana na mila na desturi zisizo rafiki pamoja na rasilimali watu wenye mafunzo na uzoefu wa kutosha katika kumlinda mtoto.
Dkt.Titus Kaniki akichangia mada wakati wa kikao kazi
Kizito ameeleza huduma mbalimbali wanazohitaji watoto wanapofanyiwa ukatili ni pamoja na afya,matibabu, sharia, malezi, ushauri nasihi, elimu na ulinzi na amewataka wajumbe kuwahamasisha jamii kuwa walinzi wa watoto kwani mtazamo wa kijamii mtoto akifanyiwa ukatili mara nyingi anasemwa vibaya na wengine wanatengwa.
Wambura L. Kizito Mratibu wa Ustawi (M) akitoa mada wakati wa kikao kazi
Katika utekelezaji  Mahakama na jeshi la polisi wanapaswa kujengewa uwezo wa namna bora za kumhudumia mtoto kwani kuna hitaji kuangalia umri na jinsi yake. Hivyo wajumbe wote waliohudhuria mafunzo hayo wametengeneza timu ambayo itahakikisha usimamiaji wa ulizi na usalama wa mtoto, utoaji wa taarifa, elimu na uhamasishaji wa kumlinda na kumthamini mtoto dhidi ya ukatili.


Uzinduzi wa Ugawaji wa Vitambulisho vya Taifa kwa watumishi wa Serikali Ukerewe.

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Estominh F. Chang'ah akipokea kitambulisho cha Taifa kama ishara ya Uzinduzi wa ugawaji wa vitambulivyo hivyo akiwa na Shahidu D. Mrabyo.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Estominh F. Chang’ah amezindua rasmi zoezi la ugawaji wa vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa watumishi wote wa Serikali walio andikishwa Wilayani Ukerewe. Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi mkubwa wa Halmashauri ambapo amepongeza zoezi limefanikiwa kwa asalimia 97%. Kitambulisho kitarahisha huduma mbalimbali na kuongeza maendeleo na kupunguza urasimu na itasaidia hata kwa watumishi watakao hitaji mikopo ya kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo. 

Shahidu D. Mrabyo Afisa Msajili (W) akiongea na watumishi wakati wa Uzinduzi
Shahidu D. Mrabyo Afisa Msajili (W), ameeleza kuwa zoezi la uandikishaji lilianza tarehe 3/4/2016 na Katika zoezi hilo jumla ya watumishi waliotakiwa kusajiliwa ni 3103 lakini watumishi 2932 walitambuliwa na kusajiliwa na maafisa wa NIDA kwa kushirikiana na Uongozi husika wa mashirika au Taasisi za serikali, na watumishi 81 walikua tayari wamekwisha sajiliwa sehemu mbalimbali nchini na hivyo kufanya idadi ya wanaotakiwa kuwa na vitambulisho kuwa 3013 na hivyo kufanya zoezi hili kufanikiwa kwa 97.099%.
Watumishi wa Serikali katika ukumbi wa  Halmashauri wakati wa uzinduzi 
Vitambulisho vinatengenezwa kwa awamu mbili, vitambulisho 2932 vilivyoombwa, kwa awamu ya kwanza ni vitambulisho 2519 vipo tayari kwa kugawiwa sawa na asilimia 85.91 na vilivyobaki vitakuja katika awamu nyingine.
Kitambulisho cha Taifa kina uwezo mkubwa wa kufanya kazi nyingi kwa pamoja, huko tunako elekea katika teknolojia kitatumika kama kitambulisho cha Taifa, kitatumika kupigia kura, kitatumika kama kadi ya mfuko wa hifadhi ya jamii, leseni ya udereva, passport ya kusafiria, pia itakuwa ni kadi ambayo unaweza kuhifadhia fedha na kuitumia popote kwa kuchanja tu, pia inaweza kutumika kama kadi ya kuingilia uwanjani mf. Uwanja wa Taifa, tutaweza kuitumia kupanda magari ya mwendo kasi na matumizi mengine mengi kulingana na kadri itavyokuwa inaunganishwa na mifumo mbali mbali hapa nchini.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Song'ora J.K Nyango akipongeza hatua ya ugawaji wa vitambulisho kwa Watumishi wa Serikali
Zoezi linalofuata na ambalo limekwisha anza ni uandikishaji wa wananchi wote ambapo mpaka sasa fomu za usajili zimekwisha sambazwa katika kata zote za Tarafa ya Mumbuga ambazo ni Bukongo, Nkilizya, Kagera, Nansio, Kakerege, Nakatunguru, Bukanda, Namagondo na Ngoma. Ametoa rai kwa wakazi wote wa tarafa ya Mumbuga kwenda kuchukua na kujaza fomu na kuwa na viambatanisho vingi iwezekanavyo ilikurahisisha upatikanaji wa kitambulisho, viambatanisho vinavyohitajika ili kusajiliwa ni cheti cha kuzaliwa, vyeti vya elimu, kitambulisho cha kupiga kura, kitambulisho cha bima ya afya, kitambulisho cha mfuko wa hifadhi ya jamii, TIN namba, kopi ya kitambulisho cha taifa cha mzazi.
Kuhusu mwanachi atakayepoteza kitambulisho cha Taifa atalazimika kulipia Tshs. 20,000/= kwa ajili ya kupata kingine, pia tunatarajia kuanza kusajiri wageni wanaoishi kihalali katika maeneo yetu, kwa hiyo ni vyema kama wapo wakaja kutuona kwa ajili ya kusajiliwa kama wageni.
Mrabyo amemshukuru Mkuu wa Wilaya, Kamati ya Ulinzi na Usalama, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, wakuu wa idara mbalimbali, wakuu wa taasisi mbalimbali za Serikali na watumishi wote wa Serikali Wilayani Ukerewe.
Shahidu D. Mrabyo akimkabidhi kitambulishi cha Taifa Hakimu Mfawidhi (W) Francis Kishenyi
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe na baadhi ya wakuu wa idara na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya katika picha ya pamoja.


Thursday, March 23, 2017

Wananchi watakiwa kuwa sehemu ya miundombinu bora ya Elimu.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Frank S. Bahati akizungumza na Serikali ya Kijiji,Kamati ya Shule ya Msingi Musozi na baadhi ya wazazi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Frank S. Bahati amefanya ziara ya ukaguzi wa ujenzi wa vyoo katika shule zilizokuwa zimefungwa na kuwasihi wananchi kuwa sehemu ya maendeleo ya elimu katika wilaya ya Ukerewe. Alikutana na Serikali ya kijiji na kamati za shule.


Mkurugenzi Mtendaji wa H/W  Frank S. Bahati Ukerewe akizungumza wa Wazazi na Kamati ya Shule Muhande.
Alitembelea shule tatu ambazo zinaendelea na ukamilishaji wa ujenzi vyoo ambazo ni Shule ya msingi Musozi, shule ya msingi Muhande, na shule ya msingi Malegea. Ujenzi wa vyoo upo katika hatua mbalimbali za kuridhisha ukilinganisha hali iliyokuwepo awali. Shule ya Msingi Musozi iliyopo kata ya Bukindo ujenzi ukikamilika kitakua ma matundu 14 ambapo kimegharimu shilingi 4,425,000/- ambapo fedha za wananchi ni shilingi 776,000/-, Shule ya Msingi Muhande iliyopo kata ya Murutunguru inatarajia kukamilisha matundu 16, Shule ya Msingi ya Malegea iliyopo kata ya Namagondo imekamilisha ujenzi wa matundu zaidi ya 16.

Ametoa agizo kwa Idara ya Elimu Msingi kuwa shule zote zilizofungwa walimu waandae na waanze masomo ya ziada kwa kipindi cha likizo hasa madarasa ya mitihani hii itawasaidia wanafunzi kusoma na kufidia muda uliopotea shule zilipokuwa zimefungwa. Pia amewataka Idara ya Elimu Msingi kufanya uchambuzi wa maeneo yote yenye uhitaji wa kuanzisha shule nyingine ili kukabiliana na wingi wa wanafunzi katika baadhi ya shule.

Mkurugenzi Mtendaji H/W ya Ukerewe akishiriki kazi wa ujenzi wa choo shule ya Msingi Muhande.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Frank S. Bahati  pamoja na baadhi ya watumishi wa Halmashauri wameshiriki  ujenzi wa choo katika Shule ya Msingi Muhande kwa kubeba matofali, mawe na kuchimba msingi vya vyoo hivyo pamoja na wananchi wa Muhande.

Mkurugenzi Mtendaji H/W ya Ukerewe akishiriki kazi wa ujenzi wa choo shule ya Msingi Muhande.

Bahati amewataka wananchi kuwa wazalendo na kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo na kuachana na itikadi tofauti za watu bali kujihusisha na mabadiliko ya elimu Wilayani. Shule zikiwa na upungufu wa miundombinu rafiki na muhimu kwa wanafunzi itawaweka mahali pabaya watoto hivyo jamii ijihusishe na kuwasaidia wanafunzi ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao.“Jukumu la kuleta maendeleo ya shule na elimu kiujumla sio la Serikali pekee bali ni letu wote, kila mmoja awe chachu ya mabadiliko”, alisema Bahati. Wanafunzi wote wanaendelea na masomo na ukamilishaji wa ujenzi wa vyoo katika shule 11 zilizokua zimefungwa unaendelea.

Baadhi ya wazazi wakishiriki Ujenzi wa choo Shule ya Msingi Muhande

Choo kilichokamilika shule ya Msingi Malegea

Mkurugenzi Mtendaji H/W Ukerewe akiwa na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Malegea

Choo Shule ya Msingi Musozi

Thursday, March 16, 2017

Ukerewe yapiga marufuku viroba na madawa ya kulevya.

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Estominh Francis Chang'ah (wapili kushoto) akiwa na askari wa Jeshi la Polisi baada ya kukamata shehena ya viroba na madawa ya kulevya.

Wilaya  ya Ukerewe imepiga marufuku matumizi ya pombe zijulikanazo kama viroba na matumizi ya madawa ya kulevya ikiwemo bangi katika kutekeleza adhma na agizo halali la Serikali.
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Estominh F. Chang’ah ambaye ni mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama wa Wilaya kwa kushirikiana na kikosi kazi kilichoundwa cha kupambana na matumizi na biashara ya pombe aina ya Viroba, na madawa ya kulevya. 

Shehena ya pombe aina ya viroba vilivyo kamatwa

 Kikosi kazi hiko kimefanya msako na kimefanikiwa kukamata mfanyabiasha mmoja Pius Sanga  aliyekutwa na katoni 128 za pombe aina ya kiroba vyenye wastani wa gharama ya shilingi milioni 15.
Msako huo pia umewezesha kukamatwa kwa mtu mmoja anaeitwa Kulwa Deo ambaye amekutwa na misokoto 70 ya bangi na kilo moja (1) unga (madawa ya kulevya). Watuhumiwa wote wanashikiliwa na jeshi la polisi na watafikishwa mahakamani.
“Watu kwa kiasi fulani bado wanajihusisha na ulimaji wa bangi katika baadhi ya maeneo nawataka waache mara moja kwani kikosi kazi bado kinaendelea na msako katika maeneo yote ya Wilaya hadi visiwani”, alisema Chang’ah.
Shehena ya pombe aina ya viroba vilivyo kamatwa

Kuendelea kutumia viroba, bangi na dawa za kulevya ni hatari sana kwa afya ya binadamu kwani vina athari mwilini, pia ni chanzo cha ajali kwani wapo waendeshaji wa vyombo vya usafiri wa barabarani wanatumia hivyo ili kuepukana na matatizo hayo amewataka watu kutokujihusiha kwani ni kinyume na agizo halali la Serikali.
Chang’ah amewataka wananchi kuacha mara moja biashara ya viroba, bangi na dawa za kulevya kwani yeyote atakae kamatwa na kikosi kazi kinachoendelea na msako atachukuliwa hatua kali za kisheria. Ametoa rai kwa wananchi wema kushirikiana na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa kuhusu watu wanao jihusisha na bangi, dawa za kulevya na viroba.